
COVID-19 / UVIKO-19
In Swahili - Kuhusu Virusi vya Corona (UVIKO-19)
UVIKO-19 ni ugonjwa unaosababishwa na virusi jamii ya corona, virusi hivi hutoka katika kundi la vimelea vingi viletavyo homa za mfumo wa hewa mfano mafua.
Kundi la virusi vya Corona lina makabila mengi ambayo mengine bado hayajagunduliwa na mengine yalishawahi kusabababisha milipuko miaka ya nyuma kama SARS-CoV mwaka 2003 iliyoanzia Asia na mwaka 2013 MERS-CoV Iliyoanzia Saudi Arabia 2012 na kusambaa kwenye nchi zaidi ya 27.
Virusi vya UVIKO-19 ni vipya na ni tofauti na virusi vingine vya jamii hiyo, viligunduliwa Disemba ya mwaka 2019 mjini Wuhan, China na kupewa jina 2019-nCOV.
Virusi hivi vinaweza kutunzwa na baadhi ya wanyama mfano popo na ngamia na huweza kusafirishwa kwenda kwa binadamu na kusababisha maradhi.
TIBA
Ugonjwa huu bado hauna tiba sawia na magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na virusi. Ugonjwa wa UVIKO-19 hauna tiba ya moja kwa moja, mgonjwa au mhisiwa wa ugonjwa hutibiwa kulingana na dalili huku uchunguzi na ufuatiliaji wa karibu zaidi ukiendelea. Ugonjwa wa UVIKO-19 una chanjo ambazo zimethibitishwa kuwa salama.

CHANJO
CHANJO NI NINI ?
Chanjo huufundisha mfumo wa kinga wa mwili jinsi ya kutambua na kupigana na vimelea kama virusi na bakteria kabla ya maradhi kutokea. Chanjo za UVIKO-19 huandaa kinga ya mwili na kuepusha mwili kuteseka na maradhi pale mtu anapopata maambukizi. Baadhi ya chanjo huhitaji dozi 1 tu na nyingine zikihitaji dozi kadhaa kwa ufanisi zaidi ili kujenga ulinzi kamili.
Chanjo za UVIKO-19 ni salama na zina kiwango cha juu zaidi cha ufanisi na usalama. Chanjo za UVIKO-19 zimefanyiwa majaribio ya kina kabla ya kupatiwa kibali au leseni ili zitumike. Tangu zilipoanza tu kutumiwa, chanjo hizi zimeendelea kuchunguzwa na taasisi husika na kukusanya taarifa ili kuhakikisha usalama na ufanisi. Hata hivyo, kama ilivyo kwa dawa zozote, chanjo zinaweza kusababisha madhara madogo madogo kama:
Maumivu, kuvimba, au wekundu katika eneo lililodungwa sindano
Homa kiasi
Maumivu ya kichwa
Maumivu ya misuli na viungo
Dalili hizo ndogo ni za kawaida na zinapaswa kutarajiwa kadiri mwili unavyojenga kinga. Madhara mabaya sana ni nadra kutokea. Mtu yeyote anayepokea chanjo anapaswa kuelezwa kikamilifu kuhusu faida na athari. Maswali yoyote au mahangaiko yanapaswa kuzungumziwa pamoja na mhudumu wa afya.
BAADHI YA AINA ZA CHANJO ZILIZOTHIBITISHWA NA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI NI :
Johnson & Johnson
Pfizer ( BioNTech)
Moderna
AstraZeneca
TAARIFA MUHIMU - UVIKO-19
MAAMBUKIZI
Ugonjwa wa UVIKO-19 huenezwa kupitia majimaji yatokayo kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu aliye na ugonjwa huu anapokohoa au kupiga chafya. Pia kwa kugusa majimaji yanayotoka puani kwa mgonjwa, kugusa nguo/vitambaaa vilivyotumiwa na mtu aliyepata maambukizi na kugusa maeneo yaliyoguswa na mtu aliye na maambukizi.
DALILI ZA UVIKO-19
Dalili huonekana siku ya 1 hadi 14 baada maambukizi. Homa na mafua makali, kubanwa mbavu na kupumua kwa shida, kukohoa, kuumwa kichwa, vidonda kooni na maumivu ya misuli. Uwezo wa mwili kupambana na maambukizi ya corona unategemea hali ya afya na lishe. Lishe bora huimarisha kinga ya mwili na husaidia mwili kupambana na Ugonjwa
JINSI YA KUJIKINGA
Epuka kusalimiana kwa mikono au kubusiana.
Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya
Jitenge na mtu/watu wenye mafua na kikohozi au wenye historia ya kusafiri nje ya nchi ndani ya siku 14.
Nawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni kila;
Baada ya kukohoa au kupiga chafya
Baada kutumia vyombo vya usafiri vyenye watu wengi au vifaa vinavyotumika na watu wengi
kabla ya kushika uso wako
Kabla na baada ya kuandaa au kula chakula
Baada ya kutoka chooni
Baada ya kushika mnyama au kinyesi cha mnyama
UVAAJI SAHIHI WA BARAKOA
Hakikisha unanawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono (sanitizer) kabla ya kuvaa barakoa.
Hakikisha barakoa yako haina tundu au uwazi wowote na upande wenye chuma laini umekaa kwa juu.
Hakikisha barakoa imebana vizuri usawa wa pua yako. Sawazisha barakoa yako kwa kuivuta mpaka usawa wa chini ya kidevu chako.
Usishushe barakoa chini ya kidevu na kuacha pua wazi kwani itaruhusu maambukizi.
Usiguse sehemu ya nje ya barakoa kuepuka maambukizi na endapo utaigusa kwa bahati mbaya hakikisha unanawa mikono yako kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono.